Psalms 36

Uovu Wa Mwanadamu

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Mtumishi Wa Bwana)


1 aKuna neno moyoni mwangu
kuhusu hali ya dhambi ya mwovu.
Hakuna hofu ya Mungu
mbele ya macho yake.

2 bKwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno
hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.

3 cManeno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,
ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema.

4 dHata kitandani mwake hupanga hila mbaya,
hujitia katika njia ya dhambi
na hakatai lililo baya.


5 eUpendo wako, Ee Bwana, unafika hadi mbinguni,
uaminifu wako hadi kwenye anga.

6 fHaki yako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama kilindi kikuu.
Ee Bwana, wewe huwahifadhi
mwanadamu na mnyama.

7 gUpendo wako usiokoma
ni wa thamani mno!
Watu wakuu na wadogo
hujificha uvulini wa mbawa zako.

8 hWanajifurahisha katika wingi nyumbani mwako,
nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.

9 iKuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,
katika nuru yako twaona nuru.


10 jDumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe,
haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.

11 kMguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu,
wala mkono wa mwovu usinifukuze.

12 lAngalia jinsi watenda mabaya walivyoanguka:
wametupwa chini, hawawezi kuinuka!
Copyright information for SwhKC